Romans 3

Uaminifu Wa Mungu

1Basi kuna faida gani kuwa Myahudi? Au kuna thamani gani katika tohara? 2 aKuna faida kubwa kwa kila namna! Kwanza kabisa, Wayahudi wamekabidhiwa lile Neno halisi la Mungu. 3 bIngekuwaje kama wengine hawakuwa na imani? Je, kutokuamini kwao kungebatilisha uaminifu wa Mungu? 4 cLa hasha! Mungu na aonekane mwenye haki, na kila mwanadamu kuwa mwongo, kama ilivyoandikwa: “Ili uthibitike kuwa wa kweli unaponena,
na ukashinde utoapo hukumu.”

5 dIkiwa uovu wetu unathibitisha haki ya Mungu waziwazi, tuseme nini basi? Je, Mungu kuileta ghadhabu yake juu yetu ni kwamba yeye si mwenye haki? (Nanena kibinadamu.) 6 eLa hasha! Kama hivyo ndivyo ilivyo, Mungu angehukumuje ulimwengu? 7 fMtu aweza kuuliza, “Kama uongo wangu unasaidia kuonyesha kweli ya Mungu na kuzidisha utukufu wake, kwa nini basi mimi nahukumiwa kuwa mwenye dhambi?” 8 gNasi kwa nini tusiseme, kama wengine wanavyotusingizia kuwa tunasema, “Tutende maovu ili mema yapate kuja?” Wao wanastahili hukumu yao.

Wote Wametenda Dhambi

9 hTusemeje basi? Je, sisi ni bora kuwaliko wao? La hasha! Kwa maana tumekwisha kuhakikisha kwa vyovyote kwamba Wayahudi na watu wa Mataifa wote wako chini ya nguvu ya dhambi. 10 iKama ilivyoandikwa: “Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja.

11 Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu,
hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu.

12 jWote wamepotoka,
wote wameoza pamoja;
hakuna atendaye mema,
naam, hakuna hata mmoja.”

13 k“Makoo yao ni makaburi wazi;
kwa ndimi zao wao hufanya udanganyifu.”
“Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.”
14 l“Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.”
15 m“Miguu yao ina haraka kumwaga damu;
16maangamizi na taabu viko katika njia zao,
17 nwala njia ya amani hawaijui.”

18 o“Hakuna hofu ya Mungu machoni pao.”

19 pBasi tunajua ya kwamba chochote sheria inachosema, inawaambia wale walio chini ya sheria ili kila kinywa kinyamazishwe na ulimwengu wote uwajibike kwa Mungu. 20 qKwa hiyo hakuna binadamu hata mmoja atakayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo ya sheria, kwa maana sheria hutufanya tuitambue dhambi.

Haki Kwa Njia Ya Imani

21 rLakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Torati na Manabii wanaishuhudia. 22 sHaki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Isa Al-Masihi kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti, 23 tkwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 uwanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Al-Masihi Isa. 25 vYeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. 26Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Isa.

Umuhimu Wa Kuwa Na Imani

27 wBasi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La hasha, bali kwa ile sheria ya imani. 28 xKwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa njia ya imani wala si kwa matendo ya sheria. 29 yJe, Mungu ni Mungu wa Wayahudi peke yao? Je, yeye si Mungu wa watu wa Mataifa pia? Naam, yeye ni Mungu wa watu wa Mataifa pia. 30 zBasi kwa kuwa tuna Mungu mmoja tu, atawahesabia haki wale waliotahiriwa kwa imani na wale wasiotahiriwa kwa imani iyo hiyo. 31Je, basi ni kwamba tunaibatilisha sheria kwa imani hii? La, hasha! Badala yake tunaithibitisha sheria.
Copyright information for SwhKC